Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhuru bado kuzaa matunda kwa raia wa Sudan Kusini

Uhuru bado kuzaa matunda kwa raia wa Sudan Kusini

Leo ni miaka minne tangu Sudan Kusini ipate uhuru wake kutoka Sudan lakini matunda ya uhuru yamesalia ndoto kwa mamilioni ya raia wa nchi hiyo ambao kila uchao hawafahamu hatma ya maisha yao. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Sauti ya Amina)

Umoja wa Mataifa unasema kilichokuwa raha sasa ni shubiri kwani mapigano yaliyoanza mwezi Disemba 2013 yameng’oa watu Milioni Mbili kutoka kwenye makazi yao, huku zaidi ya Laki Moja na Nusu wakisaka hifadhi katika vituo vya ulinzi wa raia vya Umoja huo ikiwemo Juba na Bentiu.

Muarobaini wa mzozo huo kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa ni viongozi wa serikali na wapinzani waonyeshe ujasiri wao kwa kukataa ghasia na kuanza mazungumzo thabiti.

Akizungumzia ndoto ya matunda ya uhuru kwa wananchi wa Sudan Kusini ikiwemo maendeleo, Mkuu wa operesheni za ulinzi za Umoja wa Mataifa Herve Ladsous amesema Umoja wa Mataifa unajitahidi kwa ulinzi na usaidizi wa kibinadamu, lakini ifahamike kuwa mara baada ya uhuru serikali ilianza kupata mrahaba wa mafuta …

(Sauti ya Ladsous)

“Tunafahamu wamenunua silaha, lakini wamefanya nini kuendeleza kwa ufanisi miundombinu ya afya na mtandao wa elimu na hilo ni swali ambalo raia wa Sudan Kusini wanapaswa kuhoji serikali yao.”