Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machungu ya Sudan Kusini yamezidi sasa: Ladsous

Machungu ya Sudan Kusini yamezidi sasa: Ladsous

Wakati leo ni miaka minne tangu Sudan Kusini kujipatia uhuru wake, Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Hervé Ladsous amesema ni hali ya huzuni kubwa kwa kuwa kilichoanza kwa furaha ya kuwa taifa huru sasa ni janga kubwa.

Akihojiwa na Idhaa hii, Bwana Ladsous amesema maelfu ya watu wanateseka kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe, wanawake na wasichana wanabakwa, huduma za kibinadamu ni shida na hakuna mwelekeo wa suluhu la kisiasa hivyo akasema.

(Sauti ya Ladsous)

“Nafikiri inabainisha wajibu wa viongozi wa pande zote kwenye mzozo ni muhimu sana. Hivyo ni matumaini yangu kuwa jamii ya kimataifa itashinikiza kwa kuazimia zaidi ili kupata suluhu ya kumaliza machungu haya.”

Bwana Ladous amezungumzia pia jukumu la ulinzi wa amani sambamba na kulinda raia waliopo kwenye vituo vya muda vya Umoja wa Mataifa akisema ni changamoto kubwa kwa kuwa..

(Sauti ya Ladsous)

Na bila shaka tunafanya hilo, lakini hivyo tusingalipaswa kufanya hilo kwa muda mrefu kwa sababu ina maana kuwa wakati tunalinda kambi na vituo hivyo hatuwezi kufanya doria nyingi zaidi kama inavyotakiwa kule ambako raia wanapata vitisho zaidi. Na mara nyingi vikundi vilivyojihami vinashambuliana kupitia kambi za wakimbizi wa ndani na kusababisha hasara kubwa na wahanga ambalo ni janga lingine zaidi pindi watoto wanapokutwa katikati ya mapigano.”