Kanuni za kodi na forodha zakwamisha usaidizi Nepal:OCHA

8 Julai 2015

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA imesema taratibu za forodha na kodi zinachelewesha ufikishaji wa misaada muhimu kwa wahanga wa matetemeko ya ardhi nchini Nepal.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani baada ya ziara yake nchini humo hivi karibuni, Mkurugenzi wa Operesheni wa OCHA John Ging amesema kasi ya kuingiza misaada ya kibinadamu Nepal ni kubwa lakini kuondoa misaada hiyo uwanja wa ndege Kathmandu na kupitisha mingine mipakani bado ni tatizo.,

Amelaumu urasimu kuwa chanzo cha vifaa hivyo ikiwemo vile vya makazi kushindwa kufikia familia Laki Moja ambazo zina mahitaji ya dharura kabla ya kuanza kwa msimu wa pepo za Mansoon.

Bwana Ging amesema fursa ya kufikia kaya hizo zilizoko maeneo ya ndani zaidi inapungua kwa kuwa msimu wa mvua utasababisha vijijini vilivyoko milimani visiweze kufikiwa.

Amesema wanatambua kuwa serikali ya Nepal imehama kutoka usaidizi wa dharura na sasa ni ujenzi wa kudumu lakini hatua hiyo isigharimu uhai wa wale ambao bado wana mahitaji ya dharura.

Matetemeko ya ardhi ya mwezi Aprili na Mei yalisababisha vifo vya watu zaidi ya8,800 huku makumi ya maelfu wakijeruhiwa na watu zaidi ya Milioni Mbili hawana makazi.

Changisho la kibinadamu kwa Nepal limepatiwa asilimia 46 tu ya fedha zinazotakiwa na hivyo OCHA inasihi usaidizi zaidi ili kuokoa maisha.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter