Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Myeyuko wa theluji ncha ya kaskazini unatisha: Ban

Myeyuko wa theluji ncha ya kaskazini unatisha: Ban

Wakati dunia ikijiandaa kupitisha mkataba mpya kuhusu mabadiliko ya tabianchi baadaye mwaka huu huko Paris, Ufaransa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametembelea eneo la ncha ya kaskazini ya dunia upande wa Norway na kushuhudia madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Akiwa katika chombo cha majini cha utafiti kiitwacho Lance, Ban ameshuhudia jinsi barafu katika mto wa Blomstrandbreen inavyozidi kuyeyuka kutokana na ongezeko la joto duniani na hivyo kusababisha ongezeko la kiwango cha maji ya bahari. Hivyo akasema..

(Sauti ya Ban)

" Kiwango cha maji ya bahari kinaongezeka, mito ya barafu inayeyuka haraka kuliko mwelekeo wa kawaida. Kuna hatari ya kiwanco cha asidi kwenye maji ya bahari kikaongezeka na kuathiri viumbe hai na bayonuai. Kwa hiyo ni lazima tuchukue hatua haraka kabla hatujakumbwa na majuto. Iwapo tunataka kuendeleza sayari yetu katika mazingira bora na endelevu kwa kuweka kiwango cha joto chini ya nyuzi joto mbili ni lazima tuchukue hatua."

Katika ziara hiyo Ban amekutana pia na watoto wawili wenye umri wa miaka 13 ambao wanatafiti myeyuko wa barafu kwenye eneo hilo na masuala ya tabianchi kama njia ya kushawishi binadamu kuamini athari za shughuli zao katika mabadiliko ya tabianchi.