Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sekta ya huduma yakuza uwekezaji barani Afrika:UNCTAD

Sekta ya huduma yakuza uwekezaji barani Afrika:UNCTAD

Ripoti mpya ya kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD, iliyotolewa leo imeonyesha kwamba fursa kubwa za uwekezaji barani Afrika ni katika sekta ya huduma na biashara.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, Naibu Katibu Mkuu wa UNCTAD Joakim Reiter, amesema kwamba ni dhahiri kwamba bara la Afrika ni sehemu inayozidi kuvutia uwekezaji, akiongeza kwamba si tena ukulima au madini ambayo yanavutia wawekezaji, lakini sekta ya biashara na huduma.

"Kwa hiyo kuna sura mpya ya Afrika. Na hiyo inaonekana kupitia sekta ya huduma. Kwa upande wa ajira, tayari sekta hiyo ina asilimia 32 ya ajia zote barani Afrika, na kwenye baadhi ya nchi, theluthi mbili za wafanyakazi wamejihusisha na sekta ya huduma. Na hiyo si kukaanga mikate au kutengeneza nywele”

Bwana Reiter ameeleza kwamba huduma za benki, usafiri, na utalii ni mifano ya sekta zinazokuwa kwa kasi barani humo.

Hata hivyo amesema bado changamoto zipo, akieleza kwamba ukosefu wa miongozo ya kisiasa kwa ngazi ya kitafia na kimataifa inazuia ukuaji wa sekta hiyo.

Ripoti imependekeza kuwa sekta ya huduma iwekwe kipaumbele kwenye sera za maendeleo katika ngazi ya kitaifa, na pia viwango na kanuni ziwekwe kwa ngazi ya ukanda mzima.