Hali ya haki za binadamu yazidi kuzorota Yemen

7 Julai 2015

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu imeeleza wasiwasi wake kuhusu kuzidi kuzorota kwa hali ya kibinadamu na haki za binadamu nchini Yemen, huku watu zaidi ya 1,500 wakiuawa tangu mwanzo wa mapigano, tarehe 27 Machi mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, msemaji wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Cecile Pouilly amesema mashambulizi yameendelea kwenye maeneo mbali mbali ya Yemen.

Kwa kipindi cha wiki chache zilizopita, timu yetu nchini humo imeweza kuthibitisha ukiukaji wa haki za binadamu, ukatili na ukiukaji wa haki ya kimataifa ya kibinadamu kutoka kwa pande zote za mzozo. Hizi ni pamoja na ukiukaji wa haki ya kuishi, utekaji nyara, mateso, vikwazo vya haki na uhuru wa kujieleza na kuandamana kwa amani, mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa kibinadamu, wauguzi na vituo vya afya, pamoja na waandishi na vyombo vya habari.”

Msemaji huyo amesema ofisi yake imesikitishwa na ripoti za mashambulizi dhidi ya misikiti, shule, na ofisi za Umoja wa Mataifa.

Aidha ameeleza kwamba usambazaji wa misaada ya kibinadamu unakumbwa na mapigano, huku akitoa wito kwa pande za mzozo kuheshimu haki ya kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter