Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yajikita katika kupambana na kipindupindu Sudan Kusini

UNICEF yajikita katika kupambana na kipindupindu Sudan Kusini

Wakati maradhi ya kipindupindu yanaendelea kusambaa nchini Sudan Kusini, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), amesisitiza umuhimu wa kuelimisha watoto wa shule kuhusu kinga dhidi ya maradhi hayo ambayo huathiri sana watoto.

Jonathan Veitch amesema moja ya njia muhimu za kudhibiti mlipuko wa kipindupindu nchini Sudan Kusini, ni kutoa taarifa na vifaa vinavyohitajika kwa watoto wa shule, ili waweze kujikinga pamoja na famila zao.

Amesema hayo wakati zaidi ya watu 673 wakiripotiwa kuambukizwa katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, huku idadi ya vifo ikifikia 30 na mmoja kati ya kila watano wanaokufa akiwa ni mtoto.

Katika Jimbo la Central Equatoria, ambako visa vya kwanza vya kipindupindu viliripotiwa, tayari wanafunzi 1,340 na walimu 30 wamepatiwa mafunzo ya kuokoa maisha, lego likiwa ni la kufikia shule 150.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na wadau wake likiwamo Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na Wizara ya Afya ya Sudan Kusini, wanajitahidi kutia mashule kwenye mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya mlipuko huo.