Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sheria mpya ya usalama China inatia wasiwasi- Kamishna Zeid

Sheria mpya ya usalama China inatia wasiwasi- Kamishna Zeid

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein, ameelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu sheria mpya kuhusu usalama wa kitaifa nchini China iliyopitishwa mnamo Julai mosi, na athari zake kwa haki za binadamu.

Sheria hiyo mpya inajumuisha masuala mengi mno, yakiwemo mazingira, ulinzi, fedha, teknolojia ya habari, utamaduni, itikadi, elimu na dini, huku ikielezea usalama wa kitaifa kwa njia pana mno, kama hali ambapo serikali ya nchi, uhuru, umoja, mipaka yake, hali ya watu wake na maendeleo endelevu ya uchumi na jamii yake na matakwa mengine ni salama, na havikumbani na vitisho vya ndani na nje.

Kamishna Zeid amesema sheria hiyo inaacha wazi milango ya kubinya haki na uhuru wa raia wa Uchina hata zaidi, na kukaza hata zaidi udhibiti wa mashirika ya kiraia nchini humo kuliko hali ilivyo sasa.

Amesema sheria za usalama wa kitaifa zinapaswa kuweka dhahiri ni nini kinachoweza kuchukuliwa kama kitisho kwa nchi, na njia za kukabiliana na kitisho kama hicho kwa njia ya haki, pamoja na kuwaandaa watu kwa matokeo ya vitendo vyao.