Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mratibu wa UM atoa wito kasi ya ukwamuaji wa Gaza iongezwe

Mratibu wa UM atoa wito kasi ya ukwamuaji wa Gaza iongezwe

Mwaka mmoja baada ya kuchacha mapigano huko Gaza, Mratibu wa masuala ya kibinadamu katika maeneo ya Palestina yaliyokaliwa, Robert Piper, ameelezea kuendelea kutiwa wasiwasi na hali ya kibinadamu na mwendo wa pole katika ukarabati wa Ukanda huo wa Gaza.

Bwana Piper amesema Gaza bado imo matatani, huku raia wakiathiriwa zaidi, kufuatia mkutano wa mashirika ya kibinadamu uliofanyika kwenye mji wa Gaza hapo jana Jumatatu.

Wakati wa kongamano la wahisani mnamo Oktoba 2014 mjini Cairo, wahisani waliahidi kuchangia dola bilioni 3.5 kusaidia juhudi za ukwamuaji wa Gaza. Licha ya juhudi zilizofanywa kufikia sasa, watu 100,000 bado hawana makazi, na wanaishi katika makazi ya muda, huku watu 120,000 wakiwa bado wanasubiri kuunganishwa tena kwenye mtandao wa huduma za maji mjini Gaza.

Mapigano hayo ya siku 51 yaliacha hasara ya moja kwa moja na aina nyingine yenye gharama ya dola bilioni 1.4, huku Gaza ikipata hasara ya dola bilioni 1.7 kiuchumi. Raia 1,462 waliuawa, wakiwemo watoto 551, huku maelfu yaw engine wengi wakijeruhiwa Gaza. Waisraeli sita walikuwa wahanga wa mzozo huo.