Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon azindua mfuko maalum kwa ajili ya elimu

Ban Ki-moon azindua mfuko maalum kwa ajili ya elimu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha leo uzinduzi wa Kamisheni ya Ufadhili wa Elimu duniani, itakayongozwa na waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, Gordon Brown ambaye pia ni Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu kuhusu elimu. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Uzinduzi huo umetangazwa leo wakati wa Kongamano la Elimu kwa Maendeleo linalofanyika mjini Oslo, nchini Norway, ambapo Bwana Ban ameeleza kuwa Kamisheni hiyo itasaidia katika juhudi za kuongeza ufadhili kwa ajili ya elimu, na pia katika uratibu wa ufadhili huo.

Akishukuru washindi wa tuzo ya amani ya Nobel Malala Yousafzai na Kailash Satyarthi kwa mchango wao katika kuendeleza haki ya watoto wote ya kupata elimu, Katibu Mkuu amezingatia umuhimu wa elimu kwa wote:

“ Hakuna nguvu zaidi dhidi ya msimamo mkali kuliko msichana mwenye kitabu. Mamilioni ya wasichana wanalazimika kuolewa na kuacha shule. Mamilioni ya watoto walazimika kuacha shule na kufanya kazi mashambani au viwandani. Kupigania elimu kwa wote kunalazimu kupambana na utumikishwaji wa watoto na biashara haramu ya watoto.”

Hata hivyo amemulika umuhimu wa kuwapatia elimu watoto waliopo vitani, akisikitishwa na kuona kwamba ni asilimia mbili tu ya misaada ya kibinadamu ndiyo inayofadhili elimu.