Miaka 4 ya uhuru Sudan Kusini: mgogoro na wakimbizi milioni 2.25

7 Julai 2015

Nchini Sudan Kusini, wakati maadhimisho ya miaka minne ya uhuru yakikaribia wiki hii mnamo Alhamis Julai 9, idadi ya wakimbizi wa nje na ndani ya nchi imeendelea kupanda.

Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, kufikia sasa, zaidi ya watu 730,000 wamekimbilia nchi jirani, huku milioni 1.5 wakiwa wakimbizi wa ndani. Halikadhalika, Sudan Kusini inaendelea kupokea wakimbizi kutoka nchi jirani ya Sudan, ikiwa sasa na wakimbizi wapatao 250,000, hususan kutoka majimbo ya Sudan ya Blue Nile na Kordofan Kusini.

Adrian Edwards ni msemaji wa UNHCR, Geneva

Kuna shinikizo kubwa kwa raia nchini humo, na tumeona kuongezeka kwa machafuko hivi karibuni kukisababisha watu wengi zaidi kuhama katika wiki chache zilizopita. Ukizingatia pia kuwa, ufadhili uliopo kwa Sudan Kusini sasa, ni haba mno. Asilimia 13 ni chini mno kuliko kinachohitajika

Vita vya wenyewe kwa wenyewe viliibuka nchini Sudan Kusini mnamo Disemba 2013, na kufikia sasa juhudi za kisiasa zimeshindwa kuumaliza mgogoro huo, huku hatma ya watu walioathiriwa ikiwa bado mashakani.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter