Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban atoa tamko kuhusu ripoti ya uchunguzi wa kifo cha Dag Hammarskjold

Ban atoa tamko kuhusu ripoti ya uchunguzi wa kifo cha Dag Hammarskjold

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon ametangaza leo kuwa ameipeleka ripoti ya uchunguzi, pamoja na maoni yake kuhusu hatua zilizopigwa katika kutafuta ukweli kuhusu kifo cha Katibu Mkuu wa zamani, Dag Hammarskjold, pamoja na watu 15 waliokuwa wakisafiri naye.

Akitangaza hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari, Msemaji wa Katibu Mkuu, Farhan Haq amesema barua ya Katibu Mkuu na kwa mkuu wa jopo la uchunguzi, imewasilishwa pia kwa nchi wanachama, na kuwekwa wazi kwa umma.

Bwana Haq amesema jopo hilo la uchunguzi limepiga hatua muhimu katika kutafuta ukweli kuhusu matukio ya tarehe 17 na 18 Septemba mwaka 1961, akitaja baadhi ya mambo muhimu zaidi katika ripoti hiyo ya uchunguzi..

“Jopo lilipata taarifa mpya ambazo zinathibitisha uchunguzi wa awali uliofanyiwa miili ya abiria 16 waliokuwa kwenye ndege hiyo aina ya SE-BDY. Jopo pia lilichunguza na kutathmini thamani ya taarifa mpya zinazohusiana na dhana tofauti kuhusu sababu za ajali ya ndege. Ilipata kuwa taarifa kuhusu utekaji na hujuma, hazikuwa na thamani yoyote au zilikuwa hafifu.”

Amesema pia pia jopo hilo lilipata taarifa mpya zenye dhana kuwa huenda ndege hiyo ilitunguliwa huenda ina ukweli fulani kuhusu sababu ya ajali hiyo.

“Kutokana na matokeo haya ya uchunguzi, Katibu Mkuu anaona kwamba ingekuwa vyema kufanya uchunguzi zaidi, ili kupata ukweli kamili. Hata hivyo, uchunguzi kama huo ungekuwa bora iwapo unaweza kufikia ushahidi kamili kuhusu matukio hayo ya janga ya tarehe 17 na 18 Septemba 1961, na iwapo jopo hilo litapata maelezo kamili linaloomba kutoka kwa nchi wanachama husika.”

Amesema pia Katibu Mkuu atafuatilia maombi yaliyofanywa na jopo la uchunguzi kwa nchi wanachama, ili ziliwasilishe taarifa zilizoombwa kuhusu mazingira ya kifo cha Bwana Dag Hammarskjold na maafisa wengine waliokuwa naye.