Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya hatari kubwa, kipindupindu chaweza kudhibitiwa-WHO

Licha ya hatari kubwa, kipindupindu chaweza kudhibitiwa-WHO

Kipindupindu na tishio la mlipuko wake, imetajwa kuwa changamoto kwa afya ya umma katika nchi nyingi na kwa jamii ya kimataifa, wakati ugonjwa huo ukitajwa kuwepo katika nchi mbali mbali zikiwemo Tanzania, Sudan Kusini, Haiti, Nepal na Yemen kulingana na Shirika la afya duniani WHO.

Kulingana na Dkt. Dominique Legros, ambaye anasimamia  kitengo cha kipindupindu cha WHO, matumizi ya chanjo dhidi ya kipindupindu ni chombo muhimu katika kupambana na ugonjwa huo, kama ilivyodhihirika nchini Sudan Kusini.

“Tuliamua kutoa chanjo kwa watu waliofurushwa makwao lakini kwa mfano mji mkuu Juba hatukuweza kutoa chanjo kwa watu wote kwa sababu ya idadi kubwa ya watu na uhaba wa chanjo kwa hiyo tulitoa chanjo kwa watu waliokuwa hatarini zaidi na wakati mlipuko wa kipindupindu uliibuka, kambini kulikuwa hakuna maambukizi.

Kulingana na takwimu za WHO kuna visa vipya vinavyoshuhudiwa ambako nchini Haiti mwaka huu wa 2015 kufikia mwezi Juni visa 17, 812 ikiwemo vifo 150 vimeripotiwa. Nchini Tanzania, tangu kuzuka kwa mlipuko mwezi Mei mwaka huu, vimeripotiwa visa 4711, ikiwemo maambukizi ya waTanzania 182 yaliyochechewa na uhamiaji. Nchini Sudan Kusini kufikia mwezi Julai mwaka huu visa 632 vimeripotiwa ikiwemo vifo 30.