Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamisheni kuhusu ubora wa vyakula yakutana Geneva

Kamisheni kuhusu ubora wa vyakula yakutana Geneva

Kamisheni ya kimataifa kuhusu viwango vya kimataifa vya ubora wa chakula inakutana mjini Geneva, Uswisi, kuanzia leo hadi Julai 11, ikitarajiwa kuwa nchi wanachama zitapitisha mwongozo wa viwango wastani vya usalama na ubora wa chakula. Taarifa kamili na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Miongoni mwa mambo yanayomulikwa ni udhibiti wa matumizi ya dawa katika wanyama wanaofugwa kwa minajili ya chakula au kuzalisha chakula.

Mengine yatahusu uamuzi kuhusu viwango vya juu zaidi vya madini ya risasi katika matunda na mboga mboga, viwango salama vya matumizi ya dawa za kuua wadudu pamoja na mwongozo wa kudhibiti minyoo katika nyama.

Kamisheni hiyo pia inatarajiwa kuunga mkono mfuko wa dola milioni 3.3 kila mwaka, ambao utazinduliwa na Shirika la Chakula na Kilimo FAO, na Shirika la Afya Duniani, WHO, kwa lengo la kusaidia nchi zinazoendelea kushiriki kikamilifu katika uwekaji wa viwango vya kimataifa vya chakula kati ya 2016 na 2026.