Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yakanusha madai ya upendeleo wa kikabila kwa wakimbizi wa ndani Sudan Kusini

UNMISS yakanusha madai ya upendeleo wa kikabila kwa wakimbizi wa ndani Sudan Kusini

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini umekanusha taarifa za ubaguzi wa kikabila na kisiasa wakati wa operesheni za ulinzi wa raia ulioripotiwa na gazeti moja mjini Juba.

Kwa mujibu wa UNMISS ripoti hiyo imemnukuu mkimbizi mmoja wa ndani katika kituo cha ulinzi wa raia cha Malakal  jimboni Upper Nile akishutumu walinda amani wa UNMISS kutochukua hatua yoyote wakati kituo hicho kiliposhambuliwa jioni ya Julai mbili.

Hata hivyo ujumbe huo umekanusha na  kufafanua kuwa shambulio hilo lililogharimu maisha ya mkimbizi mmoja na kujeruhi wengine sita lilitokea Julai mosi na sio mbili kama ilivyoripotiwa katika gazeti hilo.

Kadhalika taarifa hiyo katika gazeti ikinukuu chanzo ambacho hakikutajwa jina imesema wafanyakazi wa UNMISS walichukua maiti ya mkimbizi aliyeuwawa lakini hawakusaidia majeruhi kambini hapo . Ujumbe huo wa UM nchini Sudan Kusini umefafanua kuwa majeruhi wote walitibiwa ipasavyo katika hospitali huko Malakal  na  katika kliniki binafsi.

UNMISS pia imekanusha taarifa za gazeti hilo kuwa inapendelea kundi mojawapo la kabila nchini humo na kusema kuwa tangu mwezi Julai mwaka 2011 ujumbe umeanzisha sera ya kutopendelea upande wowote.

Tangu kuanza kwa mgogoro nchini Sudan Kusini mwishoni mwa mwaka 2013 UNMISS imetoa ulinzi kwa raia dhidi ya vikundi vyenye silaha bila kujali ukabila, dini au masuala ya kisiasa ambapo hadi sasa inahifadhi wakimbizi wa ndani 142,000.