Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamilioni ya watoto waokolewa kwa uwekezaji mdogo

Mamilioni ya watoto waokolewa kwa uwekezaji mdogo

Zaidi ya watoto milioni 34 wameokolewa tangu mwaka 2000 kutokana na uwekezaji katika programu za afya za watoto kwa bei nafuu ambao ni dola za Kimarekani 4,205 kwa mtoto, imesema ripoti ya Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uwezeshaji wa kifedha katika malengo ya maendeleo ya milenia kwa ajili ya malaria na chuo kikuu cha Washington nchini Marekani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ambayo kupitia chuo kikuu cha Washington imeandaliwa na taasisi yake ya tathimini ya takwimu za afya IHME, uchambuzi huo ni matokeo ya ushirikiano wa watafiti wa kimataifa ambao kwa mara ya kwanza unatoa muongozo unaoruhusu serikali, watunga sera na wahisani kufuatilia uwekezaji kwa afya za watoto na kulinganisha na vifo vya kundi hilo.

Utafiti huo ambao umepewa jina "Endeleza Ushindi, Wezesha Uwajibikaji kwa Maisha ya Watoto" unatarajiwa kuchapishwa katika jarida liitwalo Lancet la Shirika la Afya Ulimwenguni(WHO) hii leo.

Viongozi wa taasisi ya IHME ya chuo kikuu cha Washington na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uwezeshaji wa kifedha katika malengo ya maendeleo ya milenia kwa ajili ya malaria wanasema kuwa tangu mwaka 2000 hadi 2014 nchi zenye kipato kidogo na cha kati zilitumia kiasi cha dola bilioni 133 katika afya za watoto huku sekta binafsi na wahisani hususani katika nchi zenye kipato cha juu zilitumia dola bilioni 73.6.