Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kikwete aweka jiwe la msingi la jengo la Mahakama za uhalifu, MICT

Kikwete aweka jiwe la msingi la jengo la Mahakama za uhalifu, MICT

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania ameweka jiwe la msingi katika eneo litakapokuwepo jengo la Umoja wa Mataifa la mfumo wa mahakama za uhalifu wa kimataifa, MICT, linalojengwa mjini Arusha.

Uzinduzi huo umeshuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwamo msaidizi maalum wa Katibu Mkuu katika masuala ya sheria D. Stephen Mathias ambaye amesema ujenzi wa jengo hilo ni kielelezo cha umuhimu mkubwa wa uwajibikaji katika haki na utawala wa sheria na sheria yenyewe.

Kwa upande wake Rais Jakaya Kikwete amesema jengo hilo ni ishara ya heshima kwa wanaume na wanawake ambao bila huruma walishambuliwa kwa sababu ya makabila yao na kwamba uwepo wa mahakama hiyo ni udhihirisho tosha wa jumuiya ya kimataifa katika kuhakikisha inaondoa ukwepaji wa sheria.

Akizungumza kuhusu ujenzi wa mahakama hiyo Msimamizi wa MICT, John Hocking, amesema unatoa ujumbe kwa mataifa kuwa ukwepaji wa sheria haukubaliki tena na uwajibikaji unahitajika bila kujali nguvu ya watekelezaji wa uhalifu au namna gani waathirika hawasaidiki.