Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Akiwa Barbados, Ban aendeleza kampeni dhidi ya ubakaji

Akiwa Barbados, Ban aendeleza kampeni dhidi ya ubakaji

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amesema mitazamo ya wanaume inapaswa kubadilishwa ili kukabiliana ipasavyo na unyanyapaa wanaokumbana nao wanawake wengi wanaokabiliwa na ukatili wa kijinsia.

Ban amesema hayo Bridgetown, Barbados leo Julai 2, kwenye hafla ya kusaini makubaliano ya ubia kati ya serikali ya Barbados na Shirika linalohusika na masuala ya wanawake katika Umoja wa Mataifa, UN Women, kwa lengo la kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake.

Katibu Mkuu amesema eneo la Karibi lina moja ya viwango vya juu zaidi vya ubakaji, nchi tatu za eneo hilo zikiwa miongoni mwa nchi 10 zilizorekodiwa kuongoza katika vitendo vya ubakaji kote duniani.

Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF, viwango vya unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto mashariki mwa Karibi unakadiriwa kuwa kati ya asilimia 20 hadi 45, ikimaanisha mtoto mmoja kati ya watano ameathiriwa.

Ban amesema makubaliano ya leo yatatoa msukumo kwa jitihada za pamoja za kutokomeza ukatili wa kijinsia, akiongeza kuwa yatawawezesha wanawake kupata haki, na kusaidia kumaliza ukwepaji sheria wa wahalifu.