Skip to main content

Ban atoa wito kwa pande za mzozo Yemen kuhusu hali ya kibinadamu

Ban atoa wito kwa pande za mzozo Yemen kuhusu hali ya kibinadamu

Wakati Umoja wa Mataifa na wadau wake wa usaidizi wa kibinadamu wametangaza kufikia kiwango cha juu kabisa cha udharura nchini Yemen, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekariri wito wake wa kusitisha mara moja mapigano nchini Yemen ambayo inakumbwa na janga la kibinadamu.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake, ameziomba pande za mzozo kusitisha mapigano mara moja hadi mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhan ili kuwezesha usambazaji wa misaada ya kibinadamu nchini kote na kufikishia watu waliokosa bidhaa muhimu kwa miezi.

Amesema wayemen 3,000 wameuawa kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita, huku wengine 14,000 wakijeruhiwa, zaidi ua watu milioni moja wakilazimika kuhama makwao na milioni 13 wakikosa uhakika wa chakula.

Bwana Ban amesisitiza kwamba pande za mzozo zinapaswa kuheshimu sheria ya kimataifa ya kibinadamu, kulinda raia na kuwezesha wahudumu wa kibinadamu kufanya kazi zao.