Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za dharura zahitajika kukabiliana na ajira za watoto Syria- UNICEF

Hatua za dharura zahitajika kukabiliana na ajira za watoto Syria- UNICEF

Mzozo wa vita na kibinadamu nchini Syria unashinikiza idadi kubwa ya watoto kujikuta wakinyanyaswa katika soko la ajira, na juhudi zaidi zinahitajika ili kubadili mwenendo huu, kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF na Shirika la Save the Children.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa nchini Syria, watoto sasa wanachangia vipato vya familia katika zaidi ya robo tatu ya kaya zilizofuatiliwa. Nchini Jordan, nusu ya watoto wa Syria ndio wanaotafuta riziki ya familia zao peke yao, huku watoto wa umri mdogo kama miaka sita wakiwa wanafanya kazi nchini Lebanon.

Watoto walio hatarini zaidi miongoni mwao ni wale wanaotumikishwa katika vita vya silaha, kunyanyaswa kingono na vitendo haramu, vikiwemo kuombaomba kwa kupangwa na usafirishaji haramu wa watoto.

Juliette Touma ni msemaji wa UNICEF Geneva, Uswisi.

 (Sauti ya Juliette)

"Lengo letu kutoka ripoti yetu ya leo ni kuweka bayana suala la ajira kwa watoto na kuangazia mambo yaliyosababisha wasiwasi wetu ikiwemo idadi kubwa ya watoto kufanya kazi kwa sababu ni lazima wafanye hivyo na katika mazingira magumu. Hawa watoto wako hatarini sana.”