Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kituo cha kuhifadhi raia cha UNMISS chashambuliwa, Ban alaani

Kituo cha kuhifadhi raia cha UNMISS chashambuliwa, Ban alaani

Kituo cha kuhifadhi wakimbizi wa ndani huko Malakal nchini Sudan  Kusini kimeshambuliwa na vikundi vya waasi hii leo na kusababisha kifo cha raia mmoja na wengine Sita wamejeruhiwa.

Kufuatia shambulio hilo kwenye kituo hicho kilicho chini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS, Katibu Mkuu Ban Ki-moon amelaani vikali akitoa wito kwa Makamu wa zamani wa Rais Riek Machar na kamanda wa vikosi vya upinzani Johnson Olony kuchunguza tukio hilo haraka na kuwawajibisha wahusika.

Ban amekumbusha pande husika katika mzozo wa Sudan Kusini wajibu wao wa kuheshimu maeneo ya UNMISS ikiwemo vituo vya kuhifadhi raia ambavyo sasa vina zaidi ya wakimbizi wa ndani 140,000.

Amesisitiza kuwa hakuna suluhu lolote la kijeshi kwenye mzozo wa Sudan Kusini na kutoa wito kwa pande husika kusitisha chuki na kuchukua hatua za msingi kulegeza misimamo yao haraka ili kushiriki mashauriano yanayoratiwa na IGAD.

Ban katika taarifa hiyo kupitia msemaji wake ametuma rambirambi kwa familia ya wafiwa na kuwatakia ahueni ya haraka majeruhi wa shambulio hilo.