Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kiwango cha udharura Yemen chafikia juu kabisa: OCHA

Kiwango cha udharura Yemen chafikia juu kabisa: OCHA

Umoja wa Mataifa kupitia ofisi yake yausaidizi wa kibinadamu, OCHA imepandisha kiwango cha udharura nchini Yemen na kuwa kiwango cha tatu ambacho ni cha juu zaidi katika udharura, kutokana na kuzidi kuzorota kwa hali ya kibinadamu na mahitaji kuongezeka kila uchao.

Hatua hiyo inafuatia kikao cha dharura cha kamati ya wadau wa umoja wa mataif wa masuala ya  usaidizi wa kibinadamu kilichoitishwa na mkuu wa OCHA Stephen O’Brien  hii leo.

Kwa mujibu wa Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq,

“Mashirika yote yamekubaliana kutangaza kiwango cha tatu cha udharura kwa kipindi cha miezi Sita, na tathmini ya awali ya hali hiyo imepangwa kufanyika Septemba.”

Ametaja hali iliyosababisha udharura kuongezwa ili kuratibu zaidi usaidizi wa kibinadamu kuwa ni..

“Karibu watu Milioni 13 hawana uhakika wa chakula, watu Milioni Tisa nukta Nne hawana huduma ya maji safi na salama na hivyo kuhatarisha kukumbwa na magonjwa ikiwemo kipindupindu. Mfumo wa afya unasambaratika kutokana na kufungwa kwa vituo karibu 160 vya afya kutokana na ukosefu wa usalama, mafuta na vifaa vingine muhimu.”

Tangu ghasia zishike kasi nchini Yemen mwezi Machi mwaka huu, watu zaidi ya 2,800 wameuawa huku 13,000 wakijeruhiwa na zaidi ya Milioni Moja wakikimbia makwao.