Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu bilioni 2.4 hawana huduma za kujisafi - UNICEF na WHO

Watu bilioni 2.4 hawana huduma za kujisafi - UNICEF na WHO

Kutokuwa na maendeleo katika utoaji huduma za kujisafi kunadhoofisha ufanisi uliopatikana katika kuhakikisha uhai wa watoto na kuongeza upatikanaji wa maji safi ya kunywa. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani, WHO na Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF, ambayo imefuatilia utimizaji wa malengo ya milenia ya upatikanaji wa maji safi na huduma za kujisafi.

Ripoti hiyo ya pamoja kuhusu maendeleo katika upatikanaji wa huduma za kujisafi na maji safi ya kunywa mwaka 2015 na tathmini yake kulingana na MDGs, imesema mtu mmoja kati ya watatu, sawa na watu bilioni 2.4 bado hawana huduma za kujisafi, idadi hiyo ikijumuisha watu 946 ambao huenda haja kubwa hadharani.

Mkuu wa kitengo cha maji katika UNICEF, Sanjay Wijesekera, amesema kuwa takwimu hizi zinaonyesha haja ya kuangazia kutokuwepo usawa katika upatikanaji huduma hizi, na kuhakikisha kuwa watu maskini zaidi wanaanza kupiga hatua kwenye mkondo upasao, ili wapate huduma hizo sambamba na watu tajiri, na kufikia lengo la kila mtu kuwa na huduma za kujisafi ifikapo mwaka 2030.