Liberia yapata kisa kipya kimoja cha Ebola:WHO

30 Juni 2015

Shirika la afya duniani, WHO limepata ripoti za kisa kimoja cha Ebola huko Liberia, ikiwa ni wiki saba baada ya nchi hiyo kutangazwa kutokuwa na maambukizi mapya ya ugonjwa huo hatari.

Msemaji wa WHO Geneva, Uswisi, Tarik Jasarevic amethibisha kuwepo kwa kisa hicho alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari siku ya Jumanne.

(Sauti ya Tarik)

“Tunachofahamu sasa ni kwamba sampuli ilichukuliwa kutoka kwa maiti moja kwenye eneo la Margibi Kaskazini mwa Liberia. Timu ya kusaidia mazishi ilikwenda kuhakikisha maiti anazikwa kwa kuzingatia kanuni zote. Na pia  kitengo kutoka idara ya ufuatiliaji kinachohusika zaidi na Ebola ambacho kiko chini ya wizara ya afya kimepeleka jopo kwa ajili ya uchunguzi.”

Bwana Jasarevic amesema kubainika kwa kisa hicho ni ishara kuwa mfumo wa ufuatiliaji unafanya kazi vizuri na kwamba ni vyema kuendelea kuwa macho.

Tangu mlipuko wa Ebola utangazwe rasmi mwezi Machi mwaka 2014, umeshakumba zaidi ya watu 27,400 ambapo kati yao 11,207 wamefariki dunia wengi wao Liberia, Guinea na Sierra Leone.

Hata hivyo visa vipya Liberia vilikoma mwezi Mei na kutangazwa rasmi huku Guinea na Sierra Leone zikiendelea kuripoti visa vipya.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud