Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamilioni ya watoto Yemen hatarini kukumbwa na utapiamlo na kuhara

Mamilioni ya watoto Yemen hatarini kukumbwa na utapiamlo na kuhara

Machafuko yanayoendelea nchini  Yemen na athari za kiafya kwa taifa hilo vimesababisha mamilioni ya watoto kuwa katika hatari ya kupatwa na magonjwa ikiwamo  utapiamlo na kuhara limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Kwa mujibu wa mkuu wa UNICEF kanda ya Mashariki ya kati na Afrika ya Kaskazini Dk Peter Salama,watoto hawapatiwi chanjo kwa sababu kadhaa ikiwamo ukosefu wa umeme kwenye vituo vya afya, ukosefu wa mafuta ya kuhifadhi ubaridi kwa vifaa vya chanjo na kuvisambaza pamoja na hofu ya kiusalama inayosababisha wazazi kushindwa kuwapeleka watoto kupata chanjo.

Amesema watoto milioni 2.6 walioko chini ya umri wa miaka 15 wako hatarini kupatwa na utapiamlo nchini Yemen ugonjwa unaosambaa kwa kasi katika maeneo yenye mizozo. Wengine milioni 2.5 wako hatarini kukumbwa na ugonjwa wa kuharisha kutokana na ukosefu wa maji salama, huduma mbaya za kujisafi na virutubisho vya chumvi vinavyokinga upungufu wa maji mwilini.

UNICEF inasema pia kuna tishio jingine kubwa ambapo zaidi ya watoto nusu milioni walioko chini ya umri wa mitano wako hatarini kupata unyafunzi katika kipindi cha miezi 12 ijayo ikiwa hali ya machafuko itaendelea. Awali kabla ya mzozo nchini Yemen watoto waliokuwa na unyafunzi walikuwa 160,000 pekee.