Ugaidi hutatiza kufurahia haki za binadamu- Pansieri

Ugaidi hutatiza kufurahia haki za binadamu- Pansieri

Naibu Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Flavia Pansieri, amesema kuwa ugaidi hutatiza kufurahia kwa haki za binadamu, kwani vitendo vya kigaidi huvuruga serikali, hudhoofisha jamii, huhatarisha amani na usalama, na kutishia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Bi Pansieri amesema hayo akilihutubia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, ambalo limekuwa na kikao cha ngazi ya juu kuhusu athari za ugaidi.

Pansieri amesema iwapo ulimwengu unataka kuushinda ugaidi, ni lazima uelewe na kukabiliana na mazingira yanayozalisha na kukuza vitendo vya kigaidi

Hili pia linahitaji kutambua uhusiano baina ya mazingira haya na kutoheshimu haki za binadamu, ufisadi, ukwepaji sheria, kutokuwa na utawala wa sheria pamoja na kutokuwa na maendeleo na matumaini ya mustakhabali wenye amani.”

Ameongeza kuwa vitendo vya kigaidi huathiri, sio tu wahanga wa moja wa kwa moja, bali pia jamaa na jamii zao kwa ujumla, kwani huenda wakaishi kwa uoga na uchungu mwingi unaotokana na mashambulizi ya kigaidi.