Wanaume nao waanza kukimbia Burundi: UNHCR
Takribani raia Elfu Kumi wa Burundi walikimbilia nchi jirani mwishoni mwa wiki kabla serikali haijafunga mipaka yake kwa ajili ya uchaguzi uliofanyika jana. Taarifa kamili na Amina Hassan.
(Taarifa ya Amina)
Hiyo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR ambalo limesema idadi kubwa ya raia hao sasa ni wanaume.
UNHCR inasema hali hiyo ni tofauti na awali ambapo wengi waliokuwa wakikimbilia nchi jirani kukwepa machafuko walikuwa wanawake na watoto na kwamba mipaka ilifungwa kwa saa arobaini na nane.
Melissa Flemming msemaji wa UNHCR Geneva, Uswisi amesema wanaume hao walilazimika kutembea muda mrefu hadi mpakani bila hata mizigo ili wasiweze kubainika na polisi au wanamgambo na kwamba sababu ya kukimbia ni..
(Sauti ya Melissa)
“Wanataja kuvunjika kwa jitihada za kutatua mzozo nchin mwao na hali ya kutoweka kwa matumaini. Wana hofu kuwa ghasia zinaweza kushika kasi wakati wa uchaguzi ambao umeanza jana na harakati za uchaguzi zitahitimishwa na uchaguzi wa Rais uliopangwa kufanyika tarehe 15 Julai. Nchini Zambia, asilimia 90 ya raia wa Burundi wanaosaka hifadhi na vijana wa kiume.”
UNHCR inasema wakimbizi wanaofika ukimbizini wanapatiwa huduma za awali kama vile vyakula vya moto na usafiri hadi vituo vya mpito na hatimaye kambini.