Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya kibinadamu Syria yazidi kuzorota: OCHA

Hali ya kibinadamu Syria yazidi kuzorota: OCHA

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa maswala ya Kibinadamu Kyung Wha Kang amewaambia wanachama wa Baraza la Usalama kwamba jitihada za jamii ya kimataifa za kutatua mzozo wa Syria hazikuzuia hali ya kibinadamu kuzorota zaidi, huku ghasia ikikwamisha usambazaji wa misaada.

Akizungumza leo wakati wa mjadala wa Baraza hilo kuhusu Syria, Bi Kang amesema kwamba pande zote za mzozo zinaendelea kukiuka haki za binadamu na haki ya kimataifa ya kibinadamu.

Amesema changamoto kubwa ni kuwafikia zaidi ya watu milioni 4 ambao wanaishi kwenye sehemu zilizozingirwa au ambazo zinafikika kwa shida, kwa sababu ya kuongezeka kwa mapigano.

Aidha, Bi Kang ambaye pia ni Naibu mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA amesema ukosefu wa usalama unakumba shughuli za mashirika ya kibinadamu.

“ Mashirika ya Kibinadamu yanajitahidi sana ili kusaidia mamilioni ya Syria wanaoathirika na mzozo huo, lakini jitihada hizo zinahitaji ufadhili. Theluthi moja tu ya wito kwa usaidizi wa kuokoa maisha nchini Syria na kwenye ukanda huo umefadhiliwa leo. Msaada wa chakula uko mashakani. Tangu mwezi Januari, WFP ilipaswa kupunguza usambazaji wa chakula kwa asilimia 30, na inatarajia kupunguza zaidi katika kipindi cha miezi mitatu ijayo kwa sababu ya uhaba wa fedha.”

Kwa mujibu wa OCHA, watu milioni 12 wanahitaji misaada ya kibinadamu nchini Syria, wakiwemo watoto milioni 5.6.