Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israel na Palestina zapinga matokeo ya ripoti kuhusu vita vya Gaza

Israel na Palestina zapinga matokeo ya ripoti kuhusu vita vya Gaza

Wawakilishi wa Israel na Palestina hawakukubali matokeo yote ya ripoti kuhusu vita vya Gaza vya 2014 iliyowasilishwa leo mjini Geneva, Uswisi.

Wamepinga ripoti hiyo wakati Baraza la Haki za Binadamu llilipokutana leo kuijadili kufuatia kuwasilishwa kwake na mwenyekiti wa Tume huru ya uchunguzi Mary McGowan Davis.

Katika hotuba yake Bi Davis amesisitiza kwamba huenda uhalifu wa kivita ulifanyika Gaza na pande zote mbili za mzozo, akikumbusha kwamba watoto 551 wamefariki dunia katika mashambulizi hayo ya makombora ambayo yalilenga raia kwenye makazi ya Gaza.

“ Kuona kwamba hakukuwa na mabadiliko kwenye mkakati au mipango ya Israel , licha ya kupewa taarifa za kutosha kuhusu kiwango cha juu cha vifo na uharibifu, ambacho kilishuhudiwa na jamii nzima ya kimataifa, inaleta maswali kuhusu uwezekano wa ukiukaji wa haki ya kimataifa ya kibinadamu na wanasiasa hawa, ambao unaweza kuwa sawa na uhalifu wa kivita.”

Akizungumza na waandishi wa habari, mwakilishi wa Israel kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Eviator Manor ameeleza kuwa amekataa kusikiliza uwasilishaji wa ripoti hiyo kwa madai kuwa haikutambua ugumu wa vita vya siku hizi.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Palestina Ibrahim Khraishi amefurahi kwamba ripoti imetambua vifo vya raia hata hivyo akisema imeshindwa kuonyesha utofauti katika pande za mzozo.

Hatimaye Bi Davis ameeleza jinsi vizuizi dhidi ya Gaza vimesababisha ukosefu wa ajira na hali ya kukataa tamaa miongoni mwa raia.