Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nashauriana na viongozi wa Afrika kuhusu Burundi: Ban

Nashauriana na viongozi wa Afrika kuhusu Burundi: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema anafuatilia na kufanya uratibu wa karibu kuhusu hali inavyoendelea nchini Burundi wakati huu ambapo serikali ya nchi hiyo imeendelea na uchaguzi wa madiwani na bunge licha ya wito wa kimataifa wa kutaka isifanye hivyo.

Ban amesema hayo jijini New York, Marekani wakati akibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kufahamu hatua gani zitafuatia baada ya Burundi kuendelea na uchaguzi bila waangalizi wa Umoja huo.

Amesema siku moja kabla ya uchaguzi alikuwa na mashauriano kwa njia ya simu na viongozi mbali mbali akiwemo Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, na mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Nkosazana Dlamini Zuma ambako alielezea wasiwasi wake kuhusu kufanyika kwa uchaguzi huo.

(Sauti ya Ban)

“Kwa kuwa UNDP na Umoja wa Mataifa tumeondoa usaidizi wetu kwenye masuala ya uchaguzi, timu yetu ya uangalizi inafuatilia mchakato wa uchaguzi wakati huu ambapo uchaguzi unaendelea. Nilisisitiza wito wangu kwa viongozi wote wa kisiasa Burundi kuzingatia maslahi mapana ya wananchi na kusuluhisha masuala ya kisiasa kwa njai ya mazungumzo ili kulinda amani na kuiamarisha maridhiano ya kitaifa.”

Akazungumzia pia usalama na kile anachofanya sasa..

(Sauti ya Ban)

“Nasisitiza pia wajibu wa serikali ya Burundi kuhakikisha chaguzi zinafanyika katika mazingira salama na pia kuhakikisha usalama na ulinzi wa waangalizi wa Umoja wa Mataifa ili wafanye kazi yao bila vitisho na manyanyaso.Hii ni kwa mujibu wa Baraza la Usalama. Hiki ndio ninachoweza kukueleza sasa. Nafuatilia kwa karibu kinachoendelea na nashauriana na viongozi wa Afrika.”

Mkutano huo na waandishi wa habari ulifanyika baada ya Katibu Mkuu kuhutubia katika kikao cha ngazi ya juu cha Baraza Kuu kuhusu mabadiliko ya tabianchi.