Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMID yakanusha madai ya kuchelewesha mpango wa kupokonya silaha

UNAMID yakanusha madai ya kuchelewesha mpango wa kupokonya silaha

Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika huko Darfur, Sudan, UNAMID umesema unatiwa wasiwasi na ripoti za hivi karibuni kwenye vyombo vya habari kuwa unakataa kwa makusudi kusaidia tume ya Sudan ya kupokonya silaha vikundi vilivyojihami na kujumuisha wanachama kwenye jamii, SDDRC.

Katika taarifa yake UNAMI imesema inatekeleza majukumu yake ya usaidizi kwa mujibuwa makubaliano ya amani ya Doha, DDPD na kwamba ombi la hivi karibuni la kusaidia kupokonya makundi ya SAF na PDF ni kinyume na kanuni zilizowekwa.

Hata hivyo UNAMID imesema pamoja na kukataa ombi hilo ilikuwa tayari kusadia wapiganaji wa zamani waliobainika kwa mujibu wa makubaliano ya Abuja alimradi tume hiyo inawasilisha orodha kamili ya wapiganaji hao wa zamani wanaopaswa kujumuishwa katika jamii, orodha ambayo hadi sasa haijawasilishwa.

UNAMID inasisitiza kuwa DDR ni mpango ambao inaupatia kipaumbele ikitoa mfano kuwa mwaka jana pekee wapiganaji wa zamani 534 walikamilishwa kwenye mpango huo na saa inaelekeza nguvu katika kushughulikia wapiganaji wa zamani wa kikundi cha LJM.

Imetoa wito kwa SDDRC kushirikiana kwa dhati kuhitimisha mpango huo wa upokonyaji silaha na kurejesha wapiganaji kwenye jamii.