Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IMO na IOM zaazimia kushughulikia janga la wahamiaji baharini:

IMO na IOM zaazimia kushughulikia janga la wahamiaji baharini:

Kufuatia majanga yanayoendelea kutokea baharini wakati wahamiaji wakiweka maisha yao rehani ili kusaka maisha bora huko Ulaya, mashirika mawili ya kimataifa yameazimia kuweka nguvu zao pamoja ili kupatia suluhu ya kimataifa hali hiyo.

Mashirika hayo lile la masuala ya bahari, IMO na lile la uhamiaji, IOM yamefikia makubaliano hayo baada ya kikao cha viongozi wao hii leo huko London Uingereza ambapo miongoni mwa vipengee sita vya makubaliano ni kueneza taarifa kuhusu athari za uhamiaji usio na kanuni na hatari ya usafiri holela baharini .

Halikadhalika wataunda jukwaa baina ya mashirika ili kubadilishana taarifa kuhusu uhamiaji mchanganyiko usio salama baharini kwa ushirikiano na taasisi nyingine zitakazokuwa tayari kuungana nao bila kusahau harakati za uokozi kwa mujibu wa kanuni za kimataifa.

Katibu Mkuu IMO Koji Suzuki na Mkurugenzi Mkuu wa IOM William Swing wamesema wamechukua hatua hiyo kwa kutambua kuwa hali ya sasa ni janga la kibinamu na linahitaji hatua thabiti za kimataifa.