Burundi yafanya uchaguzi, MENUB yazungumza
Uchaguzi wa Bunge na serikali za mitaa umefanyika leo nchini Burundi, licha ya shinikizo la jamii ya kimataifa la kutaka uhairishwe kutokana na mazingira ya kisiasa na kiusalama. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.
(Taarifa ya Priscilla Lecomte)
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kufuatilia uchaguzi nchini Burundi, MENUB umesema waangalizi wake 36 wamefanikiwa kufuatilia uchaguzi bila kutishiwa kwa usalama wao.
Msemaji wa MENUB Vladimir Monteiro, akihojiwa nami hii leo, amesema ..
« Waangalizi wetu wametembea kwenye majimbo yote ya burundi ili kufuatilia utaratibu huo na kuandaa ripoti kwa ajili ya Katibu Mkuu na Baraza la Usalama.”
Serikali ya Burundi imeshikilia msimamo wake wa kufanya uchaguzi leo tarehe 29 Juni, kinyume na mapendekezo ya timu ya uhamasishaji iliyohusisha Umoja wa Mataifa na mashirika ya kikanda, ya kuhairisha uchaguzi hadi Julai, tarehe 30.
Bwana Monteiro ameeleza msimamo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuhusu uamuzi huo.
« Katibu Mkuu amesikitishwa kwamba mapendekezo ya timu ya uhamasishaji kuhusu kuhairishwa kwa uchaguzi hayakusikilizwa, lakini anaendelea kuwaomba wadau wa Burundi waendelee kufanya kazi ili kupata suluhu kupitia mazungumzo, bila ghasia. »