Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lazima sekta za umma na binafsi zichukue hatua kupunguza viwango vya kaboni- Ban

Lazima sekta za umma na binafsi zichukue hatua kupunguza viwango vya kaboni- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesisitiza leo umuhimu wa sekta ya umma na sekta binafsi kuchukua hatua mara moja, ili kupunguza viwango vya hewa ya mkaa angani na kuuweka ulimwengu kwenye njia thabiti dhidi ya tabianchi.

Bwana Ban amesema hayo kwenye meza ya viongozi kuhusu tabianchi, mjini San Francisco kwenye jimbo la California Marekani, ambako yupo leo kwa sherehe za kuadhimisha kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu amemulika mambo matatu ambayo angependa kuona yakimulikwa, yakiwa ni kwanza, juhudi za kufadhili kupunguza hewa ya mkaa, pili, jinsi sekta binafsi inavyoweza kutumia vyema na kupanua faida za uwekezaji unaojali mazingira uliopo sasa na wa siku zijazo, na mwisho, jinsi sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na serikali na kuzichagiza ili ziafikie mkataba shirikishi, mjini Paris.

Ban amesema, tofauti na mkataba wa Kyoto, Japan, mkataba wa Paris utajumuisha wa nchi zote, na ni lazima mkataba huo utoe mwongozo unaohitajika na sekta binafsi ili zielekeze fedha na masoko katika biashara zinazozalisha kiwango cha chini cha kaboni.