Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lasikitishwa na hali inayozorota za kibinadamu Yemen

Baraza la Usalama lasikitishwa na hali inayozorota za kibinadamu Yemen

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wameelezea kusikitishwa na hali ya kibinadamu nchini Yemen, ambayo inazidi kuzorota, ikiwemo hatari ya janga la njaa.

Katika taarifa, wajumbe hao wamekaribisha marekebisho yaliyofanyiwa ombi la Umoja wa Mataifa la dola bilioni 1.6, na kuihimiza jamii ya kimataifa kuchangia ufadhili wa ombi hilo ambalo hadi sasa limefadhiliwa kwa asilimia 10 tu.

Wajumbe hao wa Baraza la Usalama wamesema wanatambua na kukaribisha juhudi za Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Yemen za kuandaa mashauriano kuhusu Yemen mjini Geneva, na kuelezea uungaji mkono wao kwa juhudi hizo.

Aidha, wametoa wito kwa pande kinzani kuhudhuria mashauriano ya siku za usoni, na kushiriki bila vikwazo na kwa roho safi, pamoja na kutatua tofauti zao kwa mazungumzo na mashauriano, kukataa ghasia kwa ajili ya malengo yao ya kisiasa, na kujiepusha na vitendo vya uchochezi vinavyoweza kuvuruga mpito wa kisiasa.

Wamekumbusha pia kuhusu maazimio ya Baraza la Usalama yanayosisitiza haja ya kuwa na mchakato wa mpito ambao ni wa amani na utulivu, na ambao ni jumuishi, ukiongozwa na WaYemeni wenyewe.