Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zerrougui aahidi kuunga mkono mwongozo wa shule salama

Zerrougui aahidi kuunga mkono mwongozo wa shule salama

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu watoto na migogoro ya silaha, Leila Zerrougui, amesema ofisi yake itaunga mkono azimio na mwongozo wa shule salama, ambao unalenga kuzilinda shule na vyuo vikuu kutokana na matumizi ya kijeshi wakati wa mizozo ya silaha.

Katika taarifa iliyotolewa kwa niaba yake kwenye Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva, Bi Zerrougui amesema ofisi yake itaendelea kupigania watoto katika mazingira ya migogoro, kwa kuzishawishi nchi wanachama kuliridhia azimio hilo, ambalo tayari limeungwa mkono na nchi wanachama 46.

Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu amesema, ingawa kuna wale wanaosema kuna mantiki ya kijeshi ya kutumia shule, serikali na makamanda wa kijeshi ni lazima waelewe madhara ambayo vitendo kama hivyo vinaleta kwa haki ya watoto kupata elimu, na hata uhai wa watoto na raia wengine walioko katika maeneo hayo.