Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IAEA na wanasayansi kubaini bakteria anayekwamisha viinilishe mwilini

IAEA na wanasayansi kubaini bakteria anayekwamisha viinilishe mwilini

Shirika la kimataifa la nishati ya atomiki, IAEA linashirikiana na wanasayansi kufahamu uelewa kati ya hali ya lishe na bakteria mmoja anayepatikana katika tumbo la binadamu.

Tafiti za awali zilionyesha kuwa bakteria huyo Helicobacter pylori anaathiri uwezo wa mwili kufyonza viinilishe muhimu kama vile madini ya Chuma na Zinki kutoka kwenye vyakula na hivyo kuzorotesha afya ya ya kati ya asilimia 80 na 90 ya watu wazima wanaokumbwa na bakteria huyo katika nchi zinazoendelea.

Cornelia Loechl ni mtaalamu wa lishe kutoka IAEA.

(Sauti ya Cornelia)

"Kwa hiyo tunavyofikiri ni kwamba uwezo wa tumbo kutoa asidi ya Gastriki inayosaidia kufyonza viinilishe muhimu unakwamishwa na bakteria huyo na hivyo kuzuia viinilishe muhimu kwenye vyakula kushindwa kuchukuliwa na mwili. Ina maana mpango mzima wa kurutubisha vyakula unakuwa hauna maana kutokana na uambukizo wa bakteria huyo.”

IAEA inasema watu walioambukizwa bakteria huyo hawaonyeshi dalili zozote lakini uwezo wa miili yao kufyonza madini muhimu unakuwa umepungua.