Ukwepaji ushuru wapaswa kudhibitiwa kwenye nchi zinazoendelea

24 Juni 2015

Ripoti kuhusu uwekezaji katika nchi za nje kwa mwaka 2014 imeonyesha umuhimu wa kupambana na ukwepaji ushuru hasa kwenye nchi zinazoendelea.

Uhusiano baina mfumo wa uwekezaji na ushuru ni mada iliyomulikwa kwenye ripoti hiyo iliyotolewa leo na kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD, ikisema kwamba kampuni kubwa zinazowekeza kwenye nchi zinazoendelea huwa zinazidi kutumia mbinu mbali mbali ili kutolipa ushuru na hivyo kuzuia nchi kupata ufadhili muhimu kwa ajili ya maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva wakati wa kuwasilisha ripoti hiyo, Katibu Mtendaji wa UNCTAD Mukhisa Kituyi amesema mabadiliko yanahitajika kwenye mifumo ya uwekezaji na ushuru ili kuhakikisha ufadhili kwa ajili ya maendeleo endelevu.

“ Ripoti yetu mwaka jana imeonyesha mahitaji makubwa yaliyopo duniani kote kwa ajili ya maendeleo endelevu na umuhimu wa uwekezaji kwenye nchi za nje ili kupunguza tofauti za uwekezaji, hasa kwenye nchi zinazoendelea. Kwa hiyo, kuimarisha mfumo wa kimataifa wa sera za uwekezaji kunapaswa kuwekwa kipaumbele.”

Aidha ripoti imeonyesha kwamba licha ya kupungua mwaka 2014 duniani kote, uwekezaji kwenye nchi zinazoendelea umefika kiwango cha juu kabisa kihistoria, china ikiwa ni nchi ya kwanza duniani kupokea uwekezaji.

Halikadhalika Bwana Kituyi amependekeza mabadiliko katika makubaliano ya uwekezaji baina nchi, ili kuimarisha ustawi na uwazi katika maswala hayo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter