Skip to main content

MINUSTAH kusaidia serikali ya Haiti kukabiliana na wimbi la wahamiaji wanaorudi kutoka Jamhuri ya Dominika

MINUSTAH kusaidia serikali ya Haiti kukabiliana na wimbi la wahamiaji wanaorudi kutoka Jamhuri ya Dominika

Idadi ya watu wenye asili ya Haiti ambao wanarudi nchini mwao kutoka Jamhuri ya Dominika imeongezeka sana wiki hii, wengi wakiwa na wasiwasi juu ya hali yao, ameeleza Sandra Honoré, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, nchini Haiti.

Hii ni kufuatia uamuzi wa Jamhuri ya Dominika kuwalazimisha wahamiaji wasiokuwa na kitambulisho kujisajili ifikapo tarehe 17, Juni.

Akihojiwa na Redio ya Umoja wa Mataifa, Bi Honoré ameongeza kwamba watu wameripoti kushawishiwa kuondoka, wengine wengi wakiamua kurudi Haiti.

Amesema kwamba MINUSTAH imezungumza na mamlaka za serikali ya Haiti na Dominika kuhusu swala hilo, na kuwa serikali ya Haiti imeunda kamati ya mshikamano wa kitaifa kwa ajili ya kukabiliana ya idadi hii kubwa ya watu wanaorudi nchini humo, na kuwapatia huduma wanazohitaji, huku akieleza kwamba MINUSTAH itasaidia serikali ya Haiti katika jitihada hizo.

Akizingatia umuhimu wa kuheshimu haki za binadamu katika swala hilo na kuzuia kutenganishwa kwa familia, ametoa wito kwa serikali ya Jamhuri ya Dominika

“ Kufukuzwa nchini kwa watu kunapaswa kufanyika kwa njia ambayo inaheshimu utu wa binadamu, haki za binadamu na haki ya kimataifa ya kibinadamu, na hakupaswi kusababisha watu wenye uraia wa Dominika na asili ya Haiti kupoteza uraia wao na hivyo kusababisha hali ambapo kutakuwa na watu wasio na utaifa.”