Skip to main content

Wakati umefika wa kuleta mabadiliko Eritrea- mtalaam wa UM

Wakati umefika wa kuleta mabadiliko Eritrea- mtalaam wa UM

Miaka ishirini baada ya kupata uhuru, Eritrea bado haijaweza kuwapatia raia wake mustakhabali huru na mwema, amesema leo Mike Smith, mwenyekiti wa Kamisheni ya Uchunguzi kuhusu haki za binadamu Eritrea.

Akiongea mbele ya kikao cha 29 cha Baraza la Haki za Binadamu, Bwana Smith amesema Eritrea inatawaliwa na uoga na uonevu, akiongeza kwamba idadi kubwa ya watu wanaoikimbia nchi hiyo ndogo, ikiwa ni takriban watu 5,000 kila mwezi, imelazimu jamii ya kimataifa kuangazia hali ya haki za binadamu nchini humo.

Bwana Smith ameeleza kwamba Kamisheni yake imewahoji zaidi ya watu 550 kwa ajili ya ripoti iliyotolewa awali mwezi Juni, ikibaini hali ya juu ya ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo.

Kwa ujumla, amesema, hakuna utawala wa sheria nchini humo, katiba ya mwaka 1997 ikiwa haijawahi kutekelezwa, na Bunge likiwa halikutani, akiongeza kwamba vijana wanalazimishwa kuandikishwa jeshini kwa muda usiojulikana, wengine zaidi ya miaka 10.

Bwana Smith amesema kwamba sasa ni wakati wa kuleta mabadiliko :

"Wakati umefika sasa ambapo serikali ya Eritrea inapaswa kuimarisha haki za binadamu kwa raia wake. Tunahitaji kuona mafanikio si maneno tu. Kamisheni inapendekeza serikali ianze kwa kutambua uwepo wa ukiukaji wa haki za binadamu na kuhakikisha uwajibikaji kuhusu hilo, ikiwemo mauaji nje ya sheria, watu kutoweka, mateso, watu kufungwa bila haki, ukatili wa kingono, na kutumikishwa watu."