Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asisitiza azma ya UM kuokoa maisha ya watu na kulinda amani

Ban asisitiza azma ya UM kuokoa maisha ya watu na kulinda amani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliyeko ziarani huko Ulaya leo amehutubia bunge  la Baraza la Ulaya akisema Umoja wa Mataifa utachukua kila hatua kuokoa maisha na kulinda amani popote pale inapowezekana.

Ban amewaeleza wabunge hao mjini Strasbourg nchini Ufaransa, kwamba changamoto dhidi ya amani zimeenea maeneo mbali mbali duniani akitolea mfano Yemen Sudan Kusini na Syria na hivyo akitaka nchi za Ulaya na Umoja wa Mataifa kushirikiana ili kulinda amani, demokrasia na mshimakamo wa kimataifa.

Amesema uhalifu wa kupindukia unaodhihirika kwenye maeneo hayo hauwezi kufumbiwa macho akisema huu ni wakati bora zaidi kuliko wakati wowote kwa Ulaya kushiriki katika kupatia suluhu ambayo ni njia mojawapo ya kukabiliana pia na janga la uhamiaji.

Katibu Mkuu pia amegusia suala la misimamo mikali inayozidi kushamiri kila uchao akisema mwezi Novemba mwaka huu Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litazindua mpango wa utekelezaji wenye lengo la kuzuia misimamo ya aina hiyo.