Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtalaam wa UM alaani babaiko la jamii ya kimataifa nchini Syria

Mtalaam wa UM alaani babaiko la jamii ya kimataifa nchini Syria

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Uchunguzi kuhusu Syria Paulo Pinheiro amesema pande zote za mzozo Syria zinalenga makusudi raia, huku jamii ya kimataifa ikishindwa kuchukua hatua thabiti.

Amesema hayo leo wakati wa kuwasilisha ripoti ya Kamisheni hiyo mbele ya kikao cha 29 cha Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva Uswisi.

Bwana Pinheiro amesema hali iliyopo sasa nchini Syria inaonyesha kwamba jamii ya kimataifa imeshindwa kutatua mzozo huo, huku mapigano yakiendelea, aidha ukiukaji wa haki za binadamu.

Amesema kurushwa kwa makombora, kuzingirwa kwa miji, hadi kutumia gesi ya klorine, kumetesa zaidi raia akiongeza kwamba mateso hayo hayatofautishi kabila wala dini.

Aidha mwenyekiti huyo amesema kwamba kulenga raia kumekuwa mkakati wa kivita, akieleza jinsi watu, hasa wanawake na watoto, wanavyokufa kwa njaa kwenye miji iliyozingirwa kama vile Yarmouk.

Huku akisema kwamba dunia nzima itaathirika iwapo vita vitaendelea nchini Syria, Bwana Pinheiro amelaani ukosefu wa ushirikiano wa jamii ya kimataifa.

“Kuendelea kwa vita ni dalili ya kushindwa kwa diplomasia. Nchi zenye uwezo zimepotosheka katika jitihada zao za kusitisha mzozo nchini Syria. Wakifiria kwamba shinikizo la kijeshi linaweza kufanikisha utaratibu wa kisiasa, wadau wa nje wamesheheneza pande husika na pesa, wanajeshi na silaha.”

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, watu 220,000 wamefariki dunia nchini Syria tangu mwanzo wa mapigano mwaka 2011.