Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujenzi wa amani huhitaji ufadhili zaidi: Eliasson

Ujenzi wa amani huhitaji ufadhili zaidi: Eliasson

Leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kumefanyika mkutano maalum wa kamisheni ya ujenzi wa amani ikiangazia umuhimu wa ufadhili kwa ajili ya ujenzi wa amani. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Akiongea kwenye uzinduzi wa mkutano huo unaofanyika kila mwaka, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson amesema ujenzi wa amani na ukarabati wa nchi baada ya mizozo ni moja ya shughuli muhimu za Umoja wa Mataifa, lakini mara nyingi hukosa ufadhili wa kutosha.

"Unavyojua, bajeti za ujumbe za Umoja wa Mataifa zinazopitishwa na Baraza la Usalama hazina ufadhili kwa ajili ya kuimarisha mamlaka za kitaifa, usalama wa kisiasa, haki za binadamu au utawala wa sheria. Kujenga mamlaka ambazo ni msingi wa amani endelevu kunaweza kuchukua muda wa kizazi kimoja. Ndio maana uwezo wa kifedha, kisiasa, kitaaluma unapswa kuendelezwa kwa muda mrefu."

Bwana Eliasson amesisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya wafadhili na wadau wanaotekeleza ujenzi wa amani, pamoja na umuhimu wa nchi husika kuimarisha mfumo wa ukusanyaji ushuru.