Skip to main content

Makubaliano ya ubia yataimarisha jamii zilizo hatarini Sahel- OCHA

Makubaliano ya ubia yataimarisha jamii zilizo hatarini Sahel- OCHA

Kamati ya kudumu ya kikanda kuhusu udhibiti wa ukame kwenye ukanda wa Sahel, (CILSS) imesaini leo makubaliano ya ubia wa kimkakati na mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa, yakilenga kuimarisha uthabiti wa jamii za Ukanda wa Sahel ambazo zimo hatarini kukumbwa na kutokuwa na uhakika wa chakula na utapiamlo. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Ukanda wa Sahel Afrika Magharibi unakabiliwa na watu walio miongoni mwa maskini zaidi duniani, huku familia zikikumbwa na matatizo ya mara kwa mara ya chakula na lishe, ambayo sasa yamezidi kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, majanga ya asilia ya mara kwa mara na migogoro inayowalazimu watu kuhamahama.

Tangu mwaka 2012, watu milioni 20 Sahel hukabiliwa na kutokuwa na uhakika wa chakula kila mwaka, huku zaidi ya watoto milioni tano chini ya umri wa miaka mitano wakiwa na utapiamlo.

Akisaini makubaliano ya leo kwa niaba ya mashirika ya Umoja wa Mataifa, Msaidizi wa Katibu Mkuu na Mratibu wa masuala ya kibinadamu kwa ukanda wa Sahel, Robert Piper, amesema kuwa familia nyingi ni dhoofu zaidi sasa kuliko zilivyokuwa miaka 20 iliyopita, akiongeza kwamba ubia huo ulioafikiwa leo utaongeza uelewa wa kile kinachobadilisha hali ya hatari kuwa majanga, na ni nani hajajiandaa vyema kukabiliana na athari majanga hayo.