Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamilioni ya watoto maskini zaidi wameachwa nyuma, licha ya dunia kupiga hatua -UNICEF

Mamilioni ya watoto maskini zaidi wameachwa nyuma, licha ya dunia kupiga hatua -UNICEF

Jamii ya kimataifa itawafeli mamilioni ya watoto iwapo haitaangazia wale ambao ni maskini zaidi katika mkakati wake mpya wa maendeleo wa miaka 15, limeonya shirika la kuhudumia watoto, UNICEF katika ripoti yake mpya.

Ripoti hiyo ambayo ndiyo ya UNICEF ya mwisho kuhusu malengo ya milenia yanayowahusu watoto, imesema kuwa licha ya ufanisi uliopatikana, kutokuwa na fursa sawa kumewaacha watoto wengi wakiishi katika umaskini, kufariki kabla hawajatimu umri wa miaka mitano, bila elimu, au wakiwa na utapiamlo wa mara kwa mara.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Anthony Lake, amesema kuwa malengo ya maendeleo ya milenia, MDGs, yameusaidia ulimwengu kupiga hatua kubwa kwa ajili ya watoto, lakini pia yameonyesha ni watoto wangapi wameachwa nyuma. Ameongeza kuwa maisha na mustakhabali wa watoto maskini zaidi ni muhimu, si tu kwa ajili yao wenyewe, lakini pia kwa ajili ya familia zao, na jamii zao.

Amesema tofauti za vipato ndani ya nchi zimewaacha watoto kutoka familia maskini zaidi wakiwa hatarini maradufu kufa wakiwa chini ya miaka mitano, au kutofikia kiwango cha chini kabisa cha kuweza kusoma kuliko watoto kutoka familia tajiri.