Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukiukaji haki kwenye gereza la Roumieh kwasikitisha: Kaag

Ukiukaji haki kwenye gereza la Roumieh kwasikitisha: Kaag

Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, Sigrid Kaag, ameeleza wasiwasi wake kuhusiana na ripoti za hivi karibuni za ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye gereza la Roumieh nchini humo.

Taarifa iliyotolewa leo imemkariri mratibu huyo akielezea umuhimu wa Waziri wa sheria nchini Lebanon achukue hatua haraka ili kushugulikia madai hayo ya ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo kuanzisha uchunguzi.

Ingawa taarifa hiyo haijataja vitendo hivyo, Kaag amesema ripoti zilizotolewa zinaibua umuhimu wa kurejelea wito wa kutekeleza mapendekezo ya mwaka 2010 kamati ndogo ya Umoja wa Mataifa kuhusu uzuiaji wa mateso na ile ya Kamati ya Umoja wa Mataifa dhidi ya mateso ya  mwaka 2014.

Bi. Kaag ameelezea kuunga kwake mkono jitihada za serikali za kumaliza ukwepaji sheria na kusisitiza utayari wa Umoja wa Mataifa kusaidia Lebanon kutekeleza wajibu wake wa kisheria kama nchi mwanachama wa mikataba ya kimataifa ya haki  za binadamu.