Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Washindi wa Tuzo ya Mandela 2015 watangazwa

Washindi wa Tuzo ya Mandela 2015 watangazwa

Washindi wa Tuzo ya Nelson Mandela wametangazwa leo hapa mjini New York. Kutufahamisha ni akina nani, huyu hapa Priscilla Lecomte

Taarifa ya Priscilla

(Sauti ya Kutesa)

Ni rais wa Baraza Kuu Sam Kutesa akitangaza washindi wawili wa tuzo ya Mandela mwaka huu, wakiwa ni Helena Ndume kutoka Namibia na Jorge Fernando Branco Sampaio wa Ureno.

Helena Ndume ni daktari wa macho, ambaye amekuwa akijikita katika kuwatibu watu wenye upofu na magonjwa ya macho nchini Namibia na katika nchi zinazoendelea.

Naye Jorge Fernando Branco Sampaio alikuwa rais wa 18 wa Ureno, na ametambuliwa kwa juhudi zake za kuendeleza uhuru, haki za binadamu, demokrasia na amani.

Tuzo hiyo inatambua mchango wa aina yake wa washindi katika kuendeleza kazi aliyotetea Mandela ya usawa wa binadamu na haki zao, kwa kuwatia moyo wale wanaosimamia misingi hiyo ambayo pia Umoja wa Mataifa unazingatia.

Tuzo hiyo ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo Juni 6 mwaka 2014, kwa azimio namba A/68/L48, na itatolewa kwa mwanamume mmoja na mwanamke mmoja, kila baada ya miaka mitano.

Sherehe ya kutoa kuwakabidhi washindi tuzo hiyo itafanyika mnamo Julai 24 kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela.