Skip to main content

Afghanistan yaangaziwa Baraza la Usalama

Afghanistan yaangaziwa Baraza la Usalama

Leo baraza la Usalama limekuwa na mjadala maalum kuhusu Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA wakati huu ambapo kundi la magaidi la Taliban limeshambulia leo bunge la Afghanistan mjini Kabul. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Akihutubia Baraza la Usalama, Mkuu wa UNAMA Nicholas Haysom amesema juhudi zimefanyika katika maswala ya uchumi, siasa na usalama nchini humo, lakini bado changamoto ni nyingi, mzozo wa kiuchumi ukizuia nchi kutekeleza mipango yake ya maendeleo na ghasia ikiwa inaongezeka.

Kwa upande wa kisiasa, amesema licha ya kuteuliwa kwa serikali mpya baada ya uchaguzi, bado mabadiliko yanahitajika katika sheria ya uchaguzi na maswala ya utawala, Bwana Haysom akitoa wito kwa mazungumzo ya amani.

“ Amani ingekuwa na matokeo makubwa mazuri juu ya uwezo wa serikali kukabiliana na changamoto zake za kiuchumi, kiusalama na kisiasa. Kwa kipindi cha muda mrefu, amani si anasa, ni lazima. Iwapo raia wa Afghanistan hawataweza kupata njia ya kuishi pamoja kwa upatanifu, mamlaka za kisiasa na za usalama za Afghanistan pamoja na uchumi wake havitakuwa endelevu." 

Wakati huo huo, UNAMA imelaani vikali shambulio lililotokea leo dhidi ya bunge la Afghanistan na kusababisha vifo na majeruhi, shabmluio ambalo kundi la Talibani limedai kuhusika nalo.