Mkuu wa UNHCR awasili Pakistan kwa ziara ya siku 3
Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, António Guterres, ameanza leo ziara ya siku tatu nchini Pakistan, kuonyesha mshikamano wa Ramadan na serikali ya nchi hiyo.
Katika ziara hiyo, Bwana Guterres anatarajiwa pia kuelezea shukrani zake kwa watu na serikali ya Pakistan, kwa ukarimu walioonyesha kwa kuwapa hifadhi wakimbizi wengi zaidi duniani kwa kipindi cha zaidi ya miaka thelathini na mitano, kulingana na maadili na desturi ya Uislamu.
Hii ni ziara ya saba ya Kamishna huyo Mkuu nchini Pakistan katika miaka kumi, akiwa Mkuu wa UNHCR.
Ziara hii itamwezesha kujionea moja kwa moja operesheni kubwa zaidi ya kuwarejesha wakimbizi nyumbani katika historia ya UNHCR, kukutana na wakimbizi wa Afghanistan, na pia kuzuru mradi mmoja wa maeneo yaliyoathiriwa na kuwepo kwa wakimbizi.
Tangu mwaka 2002, zaidi ya wakimbizi milioni 3.8 wa Afghanistan wamerudi nyumbani kutoka Pakistan, kwa msaada wa jamii ya kimataifa.