Skip to main content

Siku ya wakimbizi duniani, idadi yao yafika milioni 60

Siku ya wakimbizi duniani, idadi yao yafika milioni 60

Leo ikiwa ni siku ya wakimbizi duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema ni muhimu kutafakari mateso ya watu karibu milioni 60 waliolazimika kuhama makwao kwa sababu ya mizozo.

Katika ujumbe wake kwa siku hii, Bwana Ban amesema idadi hiyo ni ya juu zaidi kihistoria, mtu mmoja kati ya 122 akiwa ni ama mkimbizi, mkimbizi wa ndani au mtu anayeomba hifadhi.

Katibu Mkuu ameeleza kuwa mizozo inayoendelea Syria, Iraq, Ukraine, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Nigeria au Pakistan imesababisha ongezeko hilo la idadi ya wakimbizi, huku mwaka 2014, wakimbizi wapya 42,500 wakipatikana kila siku. Ameongeza kwamba kutomalizika kwa mizozo pia kunachangia kwa sababu watu wanashindwa kurudi makwao.

Akimulika swala la uhamiaji haramu kwenye bahari ya mediteranea, Bwana Ban amesema ni lazima jamii ya kimataifa ionyeshe mshikamano na watu wanaoteseka kwa sababu ya mizozo, kwa kuwapa hifadhi watu hao, akisema hawa ni binadamu ambao walikuwa na maisha ya kawaida kabla ya kukimbia.

Hatimaye Bwana Ban ametoa wito akisema: tukumbuke utu wetu, tuadhimishe stahamala na tufunguke mioyo yetu kwa wakimbizi duniani kote.